EN FR ES AR PT SW

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA

Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara la Afrika (African Continental Free Trade Area – AfCFTA Secretariat) imeandaa Mkutano wa Wanawake na Vijana katika Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika utakaofanyika tarehe 12 hadi 14 Septemba, 2022 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.

Mkutano huu unatarajiwa kufunguliwa rasmi Septemba 12, 2022 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye pia Mhamasishaji wa Wanawake na Vijana katika Biashara Barani Afrika kupitia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika. Mkutano huo utafungwa rasmi Septemba 14, 2022 na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi. 

Mkutano huo unalenga kuwakutanisha pamoja wanawake na vijana katika biashara kujadiliana, kubadilishana uzoefu na kutatua changamoto wanazokabiliana nazo katika biashara. Hii ni hatua ya kuwawezesha wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika biashara na katika mchakato wa kuanzisha Itifaki ya Wanawake na Vijana katika Biashara inayoandaliwa na Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara la Afrika kwa kushirikiana na nchi wanachama wa AfCFTA. 

Mkutano huu utaongozwa na Kauli Mbiu isemayo “Wanawake na Vijana: Injini ya ya Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika”  “Women and Youth: The Engine of AfCFTA Trade in Africa’’ ambayo inafafanua kwa usahihi jukumu kuu la wanawake katika Afrika na Uchumi wa Dunia na umuhimu wa kuwawezesha wanawake na vijana kushiriki na kutumia ipasavyo fursa za Biashara katika Eneo Huru la Biashara la Afrika  ili kuongeza ajira na kukuza uchumi imara kwa Taifa na Jamii kwa ujumla.

Mkutano huu unatarajiwa kuhudhuriwa na  washiriki wapatao 500  ambao ni  pamoja na Viongozi mbalimbali wanawake katika ngazi ya Marais, Marais Wastaafu, Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu, Wakuu wa Taasisi mbalimbali za Kimataifa, Watu Mashuhuri, Mawaziri wanaosimamia sekta za biashara na Masuala ya Jinsia na Wanawake, Vijana na Wafanyabiashara. 

Sambamba na mkutano huo, kutakuwa na maonesho ya wafanyabiashara yatakayohusisha wafanyabiashara wanawake na vijana kutoka katika nchi 55 za Afrika.

Mhe. Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dk.Ashatu Kijaji alisema, “wanawake na vijana ndio kiini cha biashara na wamekuwa chachu muhimu katika maendeleo ya uchumi duniani, hivyo wanatakiwa kujumuishwa ili kuchangamkia fursa zinazotolewa chini ya Mkataba huo.”

Akizungumza na wanahabari leo, Mheshimiwa Wamkele Mene Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya AfCFTA alisema, “Kukutana kwetu Dar si kuzungumza tu, bali ni kuchukua hatua na kuhakikisha kuwa bara zima linaelewa kuwa iwapo AfCFTA haitafanya kazi kwa wanawake, SMEs, wajasiriamali vijana: hatutafanikiwa. “

Mkutano huu wa Wanawake na Vijana katika Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika, ni mkutano wa kwanza kufanyika tangu kuanzishwa kwa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika. Hivyo, kwa ujumla, mkutano huu utatoka na mapendekezo ya Kisera na Mikakati madhubuti ya kuimarisha uwezo wa Wanawake na Vijana kutumia fursa zinazotokana na Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika.

Mkutano huo utajadili mada mbalimbali muhimu ambazo ni pamoja na:

  1. Changamoto wanazokumbana nazo Wanawake na Vijana katika biashara za Mpakani (Reflecting on Challenges Women and Youth face in Cross Border Trade in Africa);
  1. Namna ya kusaidia Wanawake na Vijana ambao ni kichocheo katika Sekta ya Ubunifu Barani Afrika (Supporting Women and Youth as Drivers of the Creative Industry in Africa);
  1. Namna ya kutumia nyenzo za Kidigitali za Biashara ili kuimarisha ushindani Wanawake na Vijana katika Soko la Eneo Huru la Afrika la Biashara (Leveraging Digital Solutions to Trade to Enhance Women’s and Youth’s Competitiveness in the AfCFTA Market);
  1. Namna ya kusaidia urasimishaji wa biashara za Wanawake na Vijana ili waweze kunufaika zaidi na Mkataba wa Eneo Huru (Women and Youth in Informal Cross Border Trade: Supporting the formalization of women and youth in trade for greater benefits under the AfCFTA);
  2. Majadiliano kuhusu Itifaki ya Wanawake na Vijana katika Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (Youth Roundtable on the AfCFTA Protocol on Women and Youth in Trade); na
  3. Kuimarisha ushirikishwaji wa Wanawake na Vijana katika masuala ya kifedha (Promoting Financial Inclusion for Women and Youth in Trade).

Asanteni sana kwa Kunisikiliza

MWISHO

ENEO HURU LA BIASHARA LA AFRIKA (AFRICAN CONTINENTAL FREE TRADE AREA-AFCFTA)

______________________________

Eneo Huru la Biashara la Afrika (African Continental Free Trade Area-AfCFTA) ni eneo Huru la Biashara lenye jumla ya nchi 55 za Afrika zenye jumla ya watu bilioni 1.2 na Pato la Taifa (GDP) la Dola za Kimarekani trilioni 3.4 ambapo Tanzania ni mwanachama. 

Eneo Huru la Biashara la Afrika (African Continental Free Trade Area-AfCFTA) ni utaratibu wa pamoja wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (African Union-AU) unaolenga kuchochea uchumi na biashara miongoni mwa nchi wanachama. Lengo hilo litafikiwa kwa kufunguliana masoko ya biashara ya bidhaa na huduma kwa kuondoleana ushuru wa forodha (tariff) na kulegezeana masharti na taratibu nyingine zisizokuwa za kiushuru. Aidha, utaratibu huo unalenga kufanya Bara la Afrika kuwa soko moja ambapo nchi hizo zitaweza kutangamanisha juhudi nyingine za mtangamano wa kibiashara na uchumi ambazo nchi wanachama wa Umoja wa Afrika zimekwishaanzisha. Matangamano hayo ni pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki (East African Community-EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sourthern African Development Community-SADC) ambayo Tanzania ni mwanachama.

Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika ulitiwa saini katika Mkutano wa 10 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika tarehe 21 Machi, 2018 Kigali, Rwanda.  Hadi sasa, jumla ya nchi 54 kati ya nchi 55 za Umoja wa Afrika zimeshasaini mkataba huo isipokuwa nchi ya Eritrea. Nchi ambazo zimeridhia Mkataba huo ni nchi 43 kati ya 54. Tanzania ni mojawapo ya nchi ambazo tayari zimesharidhia Mkataba huo. Baraza la Mawaziri lilipitisha Waraka wa kuridhiwa kwa Mkataba huo tarehe 7 Agosti 2021 na Bungeni la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likapitisha rasmi Azimio la kuridhia Mkataba huo mnamo tarehe 9 Septemba 2021. Hata ya Tanzania kuridhia Mkataba huo iliwasilishwa kwenye Kamisheni ya Umoja wa Afrika tarehe 17 Januari 2022.

Mkataba huo ulianza kufanya kazi rasmi mwezi Mei 2019, ikiwa ni siku 30 tangu kukamilika kwa takwa la kisheria la Mkataba kuridhiwa na angalau nchi 22 (asilimia 40). Hii ni kutokana na matakwa ya Ibara ya 23 ya Mkataba wa AfCFTA. Utekelezaji wa Mkataba ulizinduliwa rasmi mwezi Julai 2019 Jijini Niamey, Niger na nchi kukubaliana utekelezaji wake uanze tarehe 1 Julai 2020. Lakini utekelezaji ulichelewa kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya maeneo ya majadiliano ambayo ni pamoja na Vigezo vya Uasili wa Bidhaa (Rules of Origin) ambavyo ni muhimu katika utambuzi wa asili ya bidhaa ikiwa ni pamoja na nchi inakotokea. Hivyo, hadi sasa bado biashara haijaanza kufanyika chini ya AfCFTA.

Media Contact
Grace Khoza – Principal Communications Advisor
Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp
WhatsApp

Related Posts

More News/Articles

Subscribe to our newsletter

Get the latest News/Updates in your inbox!
X